Tuesday, September 18, 2018

HALMASHAURI YA MUFNDI IMEPOKEA WATUMISHI 54 WA SEKTA YA AFYA



Baada ya Serikali kuajiri watumishi wapya wa sekta ya Afya mnamo mwezi Julai mwaka huu, Halmashari ya Wilaya ya Mufindi imepokea jumla ya watumishi hamsini na nne (54) walitawanywa katika vituo vya Afya na Zahanati za Halmashauri ili kupunguza changamoto ya upungufu wa wataalamu wa sekta hiyo.

Watumishi ambao wameripoti na kupangiwa vituo vya kazi  ni pamoja na wauguzi ishirini na mbili (22), Matabibu ishirini na saba (27), wataalamu wa Maabara wawili (02), wataalamu wa dawa watatu (03), pamoja na Mganga  mmoja (01)

Mgawanyo wa watumishi hawa katika vituo vya Afya na Zahanati umezingatia vigezo mbalimbali kama vile kupelekwa kwenye vituo vipya, uhitaji wa watumishi katika vituo vinavyotoa au vinatarajia kutoa huduma ya upasuaji, kupangiwa vituo ambavyo vilikumbwa na upungufu  wa rasilimali watu baada ya zoezi la kuwaondoa  watumishi wenye vyeti feki, kustaafu kwa watumishi sanjari na baadhi yao kwenda kujiendeleza kitaaluma.

Aidha, baada ya mgawanyo huo hakuna kituo cha Afya wala Zahanati ya Halmashauri ambayo imefungwa kwa kukosa wataalamu wa kotoa huduma, lakini pia kwa kuwa na wataalamu wenye weledi kwenye vituo vyote, kutasadia kukidhi moja kati ya sharti muhimu la kupata fedha kutoka kwa wahisani zitakazo saidia kuendelea kuiboresha sekta muhimu ya Afya.

Halmashauri ya Wilaya ya Mufindi yenye majimbo mawili ya uchaguzi, inajumla ya Zahanati hamsini na tatu (53) pamoja na vituo vya Afya sita (06). Uongozi wa Halmashauri tunaishukuru Serikali kwa kutupatia idadi kubwa Watumishi kwa wakati mmoja.



Friday, September 7, 2018

Mkuu wa Mkoa Iringa Mhe Ally Hapi Kuzindua Kampeni ya Iringa Mpya Mufindi.


Mkuu wa Mkoa Iringa Mhe Ally Salum Hapi anataraji kufanya ziara ya kikazi katika Wilaya ya Mufindi na Halmashauri zake kuzunguka Tarafa zote kati ya tarehe 08 Septemba hadi tarehe 13 Septemba 2018.

Katika ziara hiyo Mhe Hapi atazindua rasmi maadhimisho ya mikutano ya kampeni ya “IRINGA MPYA” kwa wananchi wa Mkoa wa Iringa, maadhimisho hayo yatafanyika kesho Tarehe 08 Septemba 2018 siku ya Jumamosi katika viwanja vya COTC vilivyopo karibu na Hospitali kuu ya Mafinga Mjini Kuanzia Saa 2:30 asubuhi.

Madhimisho hayo yataambatana na Maonesho ya Wajasiriamali, Uzinduzi wa kampeni ya upimaji VVU na saratani kwa watu wote hasa wanaume, kupokea maandamano ya kikundi cha hamasa cha usafi wa mazingira, burudani mbalimbali za wasanii ikiwemo muziki wa Live band kutoka JKT Mafinga.

Aidha Mkuu wa Mkoa atatumia fursa hii ya uzinduzi kusikiliza kero za wananchi na kuzitolea majibu, yaani Mahakama ya Wananchi.

Baada ya uzinduzi Mkuu wa Mkoa ataanza ziara yake ya tarafa kwa tarafa kukagua, kuzindua na kufungua miradi ya maendeleo kufanya mikutano ya hadhara na kusikiliza kero za wananchi ambapo tarehe 9 Septemba atakuwa Tarafa ya Kasanga, tarehe 10 Tarafa ya Malangali, Tarehe 11 Tarafa ya Kibengu, Tarehe 12 Tarafa ya Sadani na Tarehe 13 Tarafa ya Ifwagi.

Mkuu wa Wilaya Mufindi Mhe Jamhuri William anawaomba wananchi wote, wafanyakazi, wakulima, wafanyabiashara kujitokeza kwa wingi kwenye uzinduzi huu wa “IRINGA MPYA” Ili kupokea na      kutekeleza dhana ya ujenzi wa Iringa Mpya kwa vitendo.