Friday, August 10, 2018

Serikali Yakabidhi Pikipiki 27 kwa Maafisa Elimu Kata Halmashaauri ya Wilaya Mufindi.

Mkuu wa Wilaya Mufindi Mhe Jamhuri David William wa kushoto akizindua pikipiki zilizotolewa na Serikali kwa ajili ya Maafisa Elimu Kata, katikati ni Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya Mufindi Mhe Festo Mgina na anyefuatia ni Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo Bw Issaya Mbenje.

Serikali kupitia Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia imekabidhi Pikipiki ishirini na saba (27) aina ya Honda kwa Maofisa elimu kata kutoka kata zote ishirini na saba (27)  za Halmashauri ya Wilaya Mufindi Mkoani Iringa.


Akizungumza mara baada ya kukabidhi Pikipiki hizo Mkuu wa Wilaya Mufindi Mhe. Jamhuri David William, amesema Pikipiki hizo zimefika kwa wakati muafaka ili kurahisisha jukumu la ufuatiliaji na usimamizi wa elimu katika Halmashauri.

“Mmepata usafiri huu ambao utachangia kutatua changamoto za kufanya kazi zenu hivyo, hatutaki kuona utoro unaendelea, hatutaki kuona mimba zinandelea hasa katika shule za sekondari, sasa hatuna sababu ni lazima tuhakikishe elimu inakua bora zaidi na ufaulu wetu kitaifa kama Halmashauri unapanda” alisema Mhe William.

Aidha, Mhe. William, ametoa wito kwa Maofisa elimu kata kuhakikisha wanazitunza Pikipiki hizo na kusisitiza kwamba usafiri huo sio kwa ajili ya kufanyia biashara ya bodaboda bali zifanye kazi iliyokusudiwa.

Naye, kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mufindi Bw. Isaya Mbenje, amesema Pikipiki hizo ni mali ya Serikali hivyo zitasimamiwa kwa mujibu wa taratibu na sheria za serikali ikiwa ni pamoja na kufanyiwa matengenezo kwenye kalakana kwa mujibu wa sheria ya manunuzi ya umma.

Kwa upande wake Ofisa Elimu Msingi Bw. Kennedy Bukagile, amesema, lengo la Pikipiki hizo ni kuwawezesha Maofisa elimu kata kutembelea shule zilizopo katika kata zao ili kufuatilia maendeleo ya utendaji kazi.  
“Mfano Ofisa elimu kata mwenye shule nyingi ni kumi (10) kwa hiyo ni rahisi sana kuzifuatilia shule zake ndani ya mwezi mmoja anaweza kuzifikia shule zote” alisema Bw. Bukagile.

Akitoa shukrani mara baada ya hafla ya makabidhiano kiongozi wa Maofisa elimu kata ambaye pia ndiye Ofisa elimu wa kata ya Ifwagi ameishukuru serikali ya awamu ya tano chini Rais Dkt. John Pombe Magufuli, kwa kuwapatia nyenzo hiyo muhimu katika utendaji kazi lakini pia akawashukuru Wabunge, Madiwani pamoja na Mkurugenzi Mtendaji kwa kuishauri vizuri serikali na hata kupatiwa usafiri huo.

Kutolewa kwa usafiri huu ni mwendelezo wa Serikali unakusudia kuiboresha sekta muhimu ya elimu, kwani mapema mwaka 2016 Serikali ilianza kutoa kiasi cha Shilingi. 250,000 kama posho ya madaraka kwa Maofisa elimu kata, wakati wakuu wa shule wakipokea 200, 000 kila mwezi.
.

HABARI KATIKA PICHA

Mkuu wa Wilaya Mufindi Mhe Jamhuri David William akikabidhi pikipiki kwa mmojaa wa Maafisa Elimu Kata

Mkuu wa Wilaya Mufindi Mhe Jamhuri William akiongea na Maafisa Elimu Kata wakati wa Makabidhiano ya Pikipiki
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya Mufindi Mhe Festo Mgina  (Kushoto) nae akitoa salamu zake za shukrani kwa serikali.
Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya Mufindi Bwana Issaya Mbeje aktoa neno kwa Maafisa Elimu Kata wakati wa Makabidhiano ya Pikipiki
Afisa Elimu Msingi (W) Bwana Kennedy C. Bukagile akiongea na Waandishi wa Habari hawapo pichani baada ya kupokea pikipiki 27 katika Halmashauri ya Wilaya Mufindi
Afisa Elimu Kata ya Ifwagi Bwana Jordan Ngogo kwa niaba yaMaafisa Elimu Kata Halmashauri ya Wilaya Mufindi akitoa Shukrani kwa  Serikali
Kaimu Kamanda Usalama Barabarani   (W) Mufindi Koplo Hassan Khatib akitoa elimu ya usalama barabarani kwa Maafisa Elimu Kata Wote Waliokabadhiwa pikipiki..




























Picha zote na Ofisi ya Habari Mawasiliano na Uhusiano Halmashauri ya Wilaya Mufindi.