Saturday, August 4, 2018

Serikali Kuajiri Walimu 2000 wa Masomo ya Sayansi : Naibu waziri Kakunda

Mhe. Naibu waziri Kakunda akizungumza na wananchi pamoja na wanafunzi wa Shule ya Sekondari Mdabulo.
Naibu Waziri Ofisi ya Rais (OR-TAMISEMI) Mhe Joseph Kakunda, amesema serikali ipo katika hatua ya mwisho kukamilisha mchakato wa kuajiri waalimu 2000 wa masomo ya sayansi ili kupunguza changamoto ya uchache wa walimu wa kada hiyo katika shule za umma nchini.
Mhe. Kakunda ameyasema hayo katika shule kongwe ya Sekondari Mdabulo, akiwa kwenye ziara ya kikazi katika Halmashauri ya Wilaya ya Mufindi, baada ya Mkuu wa shule hiyo  Bw. George Mgomba, kueleza changamoto ya uhaba wa walimu wa sayansi katika shule yake.
 “Serikali kwa mwaka huu inaendelea na mchakato wa kuajiri walimu wa sayansi wapatao 2000 hivyo, taarifa yenu naichukua mwenyewe na kuipeleka kwa Mhe. Waziri Jafo, bila shaka walimu wawili 02 mnaowahitaji katika shule yenu mtawapata na  hili nalibeba kwa ajili ya utekelezaji”  alisisitiza Waziri Kakunda
Aidha, Mhe. Kakunda ameridhishwa na majengo mapya  ya Shule hiyo iliyojengwa kwa mfumo wa “Force Account”  kwa kuzingatia maelekezo ya kitaifa baada ya kujionea madarasa na mabweni mazuri hivyo, amesisitiza utaratibu uliotumika wa kujenga kwa njia ya Force Account uendeleee hata wakati wa mradi wa ujenzi wa bwalo la chakula utakapoanza, ambapo serikali tayari imetenga Jumla ya Tsh Milioni 100 kwa shule ya Sekondari Mdabulo.
Kwa mujibu wa mkuu wa shule ya Sekondari Mdabulo Mwalimu George Mgomba, ameipongeza serikali ya awamu ya tano kwa kuwapatia Tsh milioni 259 kwa ajili ya upanuzi wa miundo mbinu ikiwemo ujenzi wa vyumba 04 vya madarasa kwa gharama ya Tsh milioni 80, ujenzi wa mabweni 02 yaliyogharimu Tsh milioni 150, Ujenzi wa vyoo Tsh milioni 11 na kuimarisha maabara kwa gharama ya Tsh Milioni 18.
Aidha, napenda kuwashukuru wadau waliosaidia na kutuchangia kukamilisha ujenzi kwa wakati, ambao ni bodi ya shule, ambayo ilichangia msitu kwa ajili ya mbao, Rural Development Organization (R. D. O) ambao walitoa mashine za kuchanganya zege kwa siku 30 bila malipo na kampuni ya china Civil Engineering Construction Cooperation (CCECC) walitoa malori ambayo yalibeba tripu 12 za mchanga bila malipo,  majengo hayo kwa sasa yanatumika toka Agosti 2017”
Shule kongwe ya Sekondari Mdabulo ilianzishwa rasmi mwaka 1984 ikiwa ni moja kati ya shule za wananchi wa Wilaya Mufindi, mwaka 1986 ilisajiliwa ikiwa miongoni mwa shule zinazomilikiwa na Mufindi Education Trust (MET), mwaka 2003 shule ilikabidhiwa rasmi Serikalini kufuatia sera ya serikali ya kila Kata kuwa na Shule ya Sekondari, tangu mwaka huo mpaka sasa Shule imeendelea kujengwa na wananchi, wadau mbalimbali, Halmashauri ya Wilaya na Serikali kuu .
Shule ya Sekondari Mdabulo ipo katika Wilaya ya Mufindi, Tarafa ya Ifwagi, Kata ya Mdabulo katika Kijiji cha Kidete umbali wa kilometa 45 kutoka makao makuu ya Wilaya Mufindi.

HABARI PICHA

 Mhe. Naibu waziri Kakunda, akiongozwa na Mkuu wa shule ya Sekondari Mdabulo kukagua madarasa na mabweni mapya yaliyojengwa Serikali