Vijana wanafunzi wanaojiunga na chama cha Skauti wametakiwa kuzingatia maadili pamoja na kufanya vizuri katika masomo yao ili wawe mfano bora kwa wanafunzi wengine sanjari na jamii kwa ujumla.
Kauli hiyo imetolewa na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mufindi, Bw. Netho Ndilitho, wakati wa hafla ya kufunga mafunzo ya Vijana wa Skauti 909 kutoka Shule za Msingi na Sekondari za Wilaya ya Mufindi yaliyofanyika katika Kata ya Mbalamaziwa Halmashauri ya Wilaya ya Mufindi.
Ndilitho amesema, Skauti sio jeshi la kwenda kufanya vurugu katika jamii, bali ni chama ambacho kimeanzishwa kwa nia ya kuisaidia jamii kwa kutanguliza maslahi ya umma na Taifa mbele.
“Kwa hiyo nendeni makawasaidie wenzenu kwa kuwa mfano bora katika jamii, lakini pia mkawe mfano bora kwenye Madarasa yenu huko, lakini pamoja na kuhudhuria mafunzo haya ya Skauti, mhakikishe mnaweka bidii katika masomo yenu, msome kwa bidii kubwa, kwani Mhe. Rais amekuwa akitoa fedha nyingi kwa ajili ya kuwasomesha ninyi bila malipo” amesema Mkurugenzi Mtendaji huyo.
Awali akisoma risala ya chama hicho, Kiongozi wa Skauti wa Wilaya ya Mufindi Kamishina Zawadi Mwakihwaja, amesema, chama kimefanikiwa kutoa mafunzo ya stadi za uokoaji, huduma ya kwanza, Afya, uzalendo, mazoezi ya ukakamavu na uvumilivu .
“Ndugu Mgeni rasmi, tunaomba kupatiwa oneo maalum la kufanyia miradi ya Skauti kama vile kupanda bustani. Mifugo na kilimo cha mazao kulingana na majira ya mwaka” aliongeza kamishina Mwakihwaja.
Jumla ya Wanafunzi 909 ambapo kati yao Wavulana ni 452 na Wasichana 457 kutoka shule za Msingi saba (07) na Sekondari thelathini na moja (31) wamehitimu mafunzo ya Skauti yaliyofanyika katika kata ya Mbalamaziwa kwa muda wa siku nne (04)
|
Ofisa Elimu Sekondari wa Halmashauri ya Wilaya ya Mufindi Bw. Mussa Ally, akizungumza kabla ya kumkaribisha Mkurugenzi Mtendaji |
|
Wanafunzi wa Shule za Msingi na Sekondari wanachama wa Skauti wakila kiapo cha uaminifu mbele ya Kamishina Skauti Wilaya |
|
Mkuu wa Chama cha Skauti Wilaya Mufindi Kamishina Zawadi Mwakihwaja akiwaapisha wanachama wa Skauti |
|
Mgeni wa heshima Mkurugenzi Mtendaji Bw. Netho Ndilitho, akikabidhi vyeti kwa wanachama 909 walioitimu mafunzo |
|
Vijana wa Skauti wakipita kwa ukakamavu mbele ya Mgeni wa heshima |
|
Mkurugenzi Mtendaji ambaye pia ndiye Mgeni wa heshima akivishwa Skafu na mmoja wa kijana wa Skauti |
|
Mkurugenzi Mtendaji Bw. Netho Ndilito kushoto, akiwa ameketi na Ofisa Elimu Sekondari kwenye moja ya sehemu maalum iliyojengwa na Skauti kwa ajili ya kupunzika baada ya kazi |
|
Mkurugenzi akikagua sehemu ambayo Skauti huitumia kupika chakula |
|
Mkurugenzi Mtendaji akitoka kukagua sehemu maalum ambayo Skauti huitumia kuoga |