Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mufindi Mhe. Festo Mgina |
Milioni 400
Kujenga, Kukarabati Kituo cha Afya Ifwagi Halmashauri ya Mufindi
Halmashauri ya
Wilaya ya Mufindi itatumia kiasi cha shilingi milioni 400 zilizotolewa na Ofisi ya
Rais -TAMISEMI, kujenga na kufanya ukarabati mkubwa wa kituo
cha Afya Ifwagi kilichopo Kata ya Ifwagi ikiwa ni utekelezaji wa mpango mkakati
wa Serikali unaokusudia kuiimarisha sekta ya Afya hususani Afya ya Mama na
Mtoto katika Halmashauri ya Mufindi.
Kwa mujibu wa Mwenyekiti
wa Halmashauri ya Wilaya ya Mufindi na Diwani wa kata ya Mninga Mhe. Festo
Mgina, amesema, fedha hizo zitatumika kukarabati na kufanya utanuzi wa Wodi ya
Wazazi, ujenzi wa jengo la upasuaji, ujenzi wa Nyumba ya Mganga sanjari na
Jengo la Maabara.
Mhe. Mgina,
amebainisha kuwa ujenzi na ukarabati huo, utatekelezwa kwa mfumo wa “Force Account” ambapo Halmashauri
hutumia Mafundi wenyeji watakao thibitishwa kuwa na weledi unaokubalika huku
wakitakiwa kutekeleza jukumu hilo kwa kipindi kisichozidi miezi mitatu chini ya
usimamizi wa karibu kutoka kwa Mhandisi wa ujenzi wa Halmashauri
“Nawahamasisha
wananchi wote wa kata ya Ifwagi, kujitolea nguvu kazi wakati wa utekelezaji wa
mradi huu muhimu kwa ustawi wa Afya zetu na Halmashauri ya Mufindi kwa ujumla”
alisema Mhe.Mgina,
Aidha, ili
kuhakikisha mradi huu unatekelezwa kwa wakati na ubora uliokusudiwa, Mkurugenzi
Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya Mufindi Profesa Riziki Shemdoe, akiwa ndiye
mtendaji Mkuu, ameunda kamati maalum yenye vikosi kazi vitatu vinavyojumuisha Maofisa kutoka idara mbalimbali pamoja na wananchi
ili kuhakikisha mradi huu unatekelezwa kwa wakati na kuzingatia viwango elekezi.
Ikumbukwe kuwa
mwishoni mwa mwaka jana Ofisi ya Rais -TAMISEMI
ilitoa kiasi kama hicho cha fedha kwa ajili ya ujenzi na ukarabati wa kituo cha
Afya Malangali kilichopo kata ya Malangali na tayari ujenzi wake umekamilika na
kinachosubiriwa ni mapokezi ya vifaa tiba vyenye thamani ya shilingi Milioni 300 kutoka bohari ya dawa (MSD)