Saturday, February 2, 2019

WAGA KUNUFAIKA, MAMILIONI YA UWINDAJI WA KITALII




Mwenyekiti wa Bodi ya WAGA Mhe. Ashery Mtono akisaini Mkataba pamoja na mwekezaji  Bw. Akram Azizi

Jumuiya ya hifadhi ya wanyamapori WAGA inayaoundwa na vijiji vitano vilivyopo kwenye Halmashauri ya Wilaya ya Mufindi, Halmashauri ya Mbalali na Halmashauri ya Iringa imetiliana saini mkataba wa uwindaji wa kitalii wenye thamani ya dola 30,000 za Kimarekani Zaidi ya shilingi 60,000,000 za Kitanzania na kampuni ya Wembere safaris inayojihusisha na shughuli za uwindaji  wa kitalii  hapa nchini.

Mkataba huo uliosainiwa mwanzoni mwa wiki hii na kushuhudiwa na wakuu wa Wilaya za Mufindi na Mbalali pamoja na wajumbe kutoka vijiji vyote vitano vinavyounda jumuya ya WAGA ambavyo ni Kijiji cha Igomaa na Ihanzutwa kwa Halmashauri ya Wilaya ya Mufindi, Nyamakuyu na Nyakadete kwa Halmshauri ya Mbalali huku Halmashauri ya Iringa ikihusisha Kijiji kimoja cha Mauninga.

Mkataba huo unamruhusu mwekezaji kufanya shughuli za uwindaji wa kitalii katika kitalu cha WAGA kwa kipindi cha miaka mitano (05) lakini pia unamtaka mwekezajia huyo kutoa kiasi cha dola 5,000 za Kimarekani sawa na Fedha za Kitanzania Zaidi ya shilingi milioni 10 zitakazotumika kustawisha maendeleo ya Vijiji hivyo.

Akizungumza mara baada ya kusaini mkataba kwa niaba ya Jumuiya, Baraza la udhamini la jumuia ambaye pia ni Diwani wa kata ya Sadani Mhe. Ashely Mtono, amemtaka mwekezaji huyo kuzingatia makubalino yaliyoainishwa katika mkataba ili kuepusha migogoro ambayo inaweza kujitokeza hapo badae endapo atakiuka makubaliano hayo.

“Nashukuru kwamba mwekezaji amekubali kilakitu kilichopo katika mkataba na sisi tumejiridhisha, lakini tumesaini leo mkataba, naomba azingatie mkataba ili mwisho wa siku mimi niliyesaini kwa niaba ya Jumuiya usije kuniingiza katika matatizo, nayasema haya kwake kwa kuwa yeye ndiye mtekelezajii na kama ni migogogro sehemu kubwa inaweza kutokea upande wake na sitegemei wala sitarajii kuwa Jumuiya inaweza kuanzisha mgogoro”

Kwa upande wake Mkurugenzi wa kampuni ya uwindaji ya Wembere Safarie Bw. Akram Aziz, amesema kampuni yake itafanya kazi kwa kuzingatia taratibu za nchi pamoja na kuheshimu makubaliano yaliyofikiwa kupita mkataba uliosainiwa na kusisitiza kuwa wao kama kampuni hawawezi kuwa kikwazo katika kutekeleza yale yote yaliyokubalika kupitia mkataba huo.

“Kwa upande wetu naahidi tutatekeleza kwa vitendo na hatutegemei wala tatutarajii kuwa na mgogolo wowote kilakitu kilichomo ndani ya mkataba kitatekelezwa kama kilivyo kwani sisi sote ni Watanzania na nia yetu ni kujenga nchi yetu ili ifikie kilele cha mafanikio “

Naye Ofisa wanyamapori wa Halmashauri ya Wilaya ya Mufindi Bi, Rachael Nhambu, amefafanua kuwa, Jumuiya za kuhifadhi Wanyamapori zinaundwa kwa mujibu wa sharia 05 ya kuhifadhi Wanyamapori ya mwaka 2019 kifungu cha 31,32 sanjari na kifungu cha 33 pamoja na kanuni ya kusimamia wanayamapori ya mwaka 2019.

 amefafanua kuwa suala la Jamii kumiliki vitalu vya wanyamapori katika maeneo yanayopakana na Hifadhi za Taifa ni kwa Mujibu wa Sheria ya wanyamapori ya Na. 05 ya mwaka 2009 ambayo inaziruhusu jamii zilizo ridhia na kutoa ardhi ambayo ingeweza kutumika kwa shughuli za kijamii kuwa wamiliki wa vitalu vya kuhifadhi wanyamapori na fedha zitakazotokana na uwekezaji huo hurudi katika Vijiji husika ili zitumike  kwa ajili ya kutekeleza na kuendeleza miradi ambayo ni kwa ajili ya maendeleo ya jamii husika.

Ameongeza kuwa Jumuiya ya WAGA imeundwa na Vijiji 05 vya Igomaa, Ihanzutwa, Nyakadete, Nyamakuyu na Mauninga baada ya Vijiji hivyo kutoa maeneo yao na kuamua kuhifadhi wanyamapori badala ya shughuli nyingine.

Zoezi la kusaini Mkataba


 
Mwekezaji na Mwenyekiti wa Bodi katika picha ya pamoja na wajumbe wa jumuiya ya WAGA