Mkuu wa Wilaya ya Mufindi Mhe. Jamhuri William kushoto, akimkabidhi Afisa wa Benki mfano wa hundi kama ishara ya kutoa Mikopo kwa Wanawake na Vijana. |
Jumla ya shilingi Milioni 100, zimetolewa kwa sharti la Mkopo kwa
vikundi vya Wanawake na Vijana wa Halmashauri ya Wilaya ya Mufindi,
ikiwa ni utekelezaji wa takwa la sheria inayozitaka mamlaka za Serikali
za mitaa nchini kutenga asilimia 10 ya mapato ya ndani kwa lengo la
kuwakopesha vijana na Wanawake ili wajiajiri kupitia shughuli za
kijasirimali hivyo kuboresha maisha yao.
Akisoma taarifa ya Mikopo hiyo, Mkuu wa Idara ya maendeleo ya jamii
Halmashauri ya Wilaya ya Mufindi Bw. Hatibu Bwashehe, ametanabaisha
kuwa, kati ya vikundi hivyo, vikundi 22 vya wanawake vimekopeshwa jumla
ya shilingi Milioni 62, wakati vikundi 15 vya Vijana vimenufaika na
Mkopo huo kwa kupata shilingi Milioni 38.
Akizungumza kabla ya kukabidhi hundi kwa walengwa, mgeni wa heshima
katika hafla hiyo Mkuu wa Wilaya ya Mufindi Mh. Jamhuri William,
amevitaka vikundi hivyo vielewe kuwa, fedha wanazopokea ni Mkopo hivyo,
zitumike kulingana na maandiko waliyowasilisha badala ya kuzitumia kwa
malengo tofauti kama vile kuchangia harusi au kununua mavazi ya kifahari
na kuongeza kuwa hatua kali za kisheria zitachukuliwa kwa kutorejesha
fedha za Serikali.
Naye Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Mufindi Mh. Festo Ngina,
amepongeza mwenendo mzuri ya urejeshaji Mikopo kwa vikundi
vilivyokopeshwa kiasi cha shilingi Milioni 300 kwa mwaka wa fedha
uliopita wa 2016 – 2017 na akaongeza kuwa ili hali ya urejeshaji izidi
kuwa bora zaidi, Watendaji wa kata na Vijiji watahusika kufuatilia
marejesho hayo kama ambavyo wanahusishwa kwenye chakato kusajili
vikundi.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Mtendaji wa wa Halmashauri ya Wilaya ya
Mufindi Profesa Riziki Shemdoe, amewahimiza Vijana na Wanawake wa
Halmashauri hiyo kuendelea kuwasilisha maombi kwa kuwa Halmashauri yake
tayari imetenga fedha nyingine kiasi cha shilingi Milioni 140 ambazo
watazikopesha baadaye mwezi ujao mara baada ya kukamilisha uchambuzi wa
maandiko ambayo yatakuwa yanalenga kuanzisha viwanda Vidogo.
Aidha, wanufaika wa Mkopo huo ambao ni Wanawake na Vijana,
wameipongeza Serikali ya awamu ya tano chini ya uongozi wa Rais John
Pombe Magufuli, kwa kuwathamini na kuwapatia mikopo hiyo huku wakiahidi
kuzitumia kwa malengo na kurejesha kwa wakati.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mufindi Prof. Riziki Shemdoe, akizungumza na Viongozi wa Vikundi vya Wanawake na Vijana wakati wa hafla ya kukabidhi hundi |
No comments:
Post a Comment