Mkuu wa
Wilaya ya Mufindi amewataka wazazi na walezi waendelee kuchangia chakula cha
mchana kwa wanafunzi wa kutwa kwa shabaha ya kuinua kiwango cha ufaulu,
kupunguza utoro pamoja na kuleta usawa miongini mwao.
Akiongea
na wananchi wa Igowole katika kilele cha wiki la kusoma lililofanyika katika Viwanja vya shule ya
Msingi Igowole iliyopo Halmashauri ya Wilaya Mufindi, Mwakilishi wa Mkuu wa
Wilaya ya Mufindi Bwana Joseph Mchina, amewataka vingozi wa serikali za vijiji
kuendelea kutekeleza mkakati wa utoaji wa chakula cha Mchana shuleni kwa kuwamasisha
wazazi kuchangia kwa mujibu wa sera ya Elimu bila malipo.
Aidha,
amewapongeza viongozi wa siasa ambao wamekuwa bega kwa bega katika kuelimisha
jamii na wazazi kuhusu umuhimu wa utoaji wa chakula cha mchana shuleni.
“Napenda
kupongeza kata zote ambazo zinazotoa chakula cha mchana kwa wanafunzi shuleni,
utoaji wa chakula cha mchana shuleni huleta usawa kati ya walionacho na wasionacho,
huimarisha mahudhurio ya wanafunzi shuleni huongeza usikivu wa wanafunzi
darasani na hutunza muda wa ratiba nzima ya shule” alisema Mchina
Akitoa
taarifa kwa mgeni rasmi, Afisa Elimu wa Halmashauri ya Wilaya ya Mufindi Bwana Kennedy
Bukagile, alisema Halmashauri ya Wilaya Mufindi imejiwekea mkakati mzuri wa
kuwapatia wanafunzi chakula cha mchana ili kuimarisha usikivu na mahudhurio shuleni,
“wazazi
wamejitoa kulima shamba la maharage na Mahindi lenye jumla ya hekari 294 kwa
ajili ya chakula cha mchana kwa wanafunzi shuleni”
Afisa
huyo mwenye dhamana ya Elimu, ameongeza kuwa, Idara yake kwa kushirikiana na
wadau mbalimbali wamewezesha kamati za shule kujengewa uwezo wa uhamasishaji na
pia kuwa na wahamasishaji jamii wa
masuala ya elimu kwa kila shule,
wakishirikiana na kamati za shule kuhakikisha kuwa wanafunzi wanapata chakula
cha mchana jambo ambalo limesabisha kuongezeka kwa ufaulu sanjari na kushuka
kwa takwimu za utoro.
Kwa upande
mwingine Maadhimisho hayo yalienda sambamba na maonesho ya mabanda ya elimu na mashindano
ya wanafunzi katika stadi za KKK, ambapo washindi wa shindano hilo walitangazwa
na kupewa zawadi na Mgeni rasmi ambapo nafasi ya kwanza ilichukuliwa na Mwanafunzi
Anania Ng’umbi, darasa la pili wa Shule ya Msingi Igowole.
Aidha “kujua kusoma na kuandika ni haki ya kila mtu jambo hilo linamsaidia mtu kuwa na uwezo na njia yenye kumuwezesha kufanya maendeleo katika maisha yake pamoja na watu wengine”, Tamko la Shirika la UNESCO
Maadhimisho ya Wiki la Kusoma yanalenga kukuza na koungeza ari ya ushindani katika kujifunza stadi za msingi za kusoma, Kuandika na Kuhesabu (KKK) Ujumbe wa wiki la elimu mwaka huu ni Stadi za KKK ni Msingi wa Elimu, tuwekeze katika Elimu kuelekea Uchumi wa Viwanda
No comments:
Post a Comment