Mkuu mpya wa Mkoa Iringa Mhe. Ally Hapi, ametoa Siku 90 kwa Halmashauri zote za Mkoa wa Iringa, Kuhakikisha wazee wote Mkoani humo wanatambuliwa na kupewa vitambulisho vya matibabu bure ili waweze kutibiwa kwenye hospitali yoyote ya umma bila usumbufu.
Mhe. Hapi, ameyasema hayo wakati akizungumza na watumishi wa umma Wilayani Mufindi katika ziara yake ya kwanza yenye lengo la kujitambulisha kwa watumishi wa umma Wilayani humo.
“Na Kwenye hili nimesema wazee wasiwafuate Halmashauri kwenda kupewa hivyo vitambulisho bali Halmashauri Kupitia DMO na timu yake mtoke muwafuate wananchi kata kwa kata muwaandikishe, Muwasajili na kisha muwapelekee vitambulisho mahali walipo na baada ya siku 90 nataka nipate mrejesho chanya kuhusu agizo hili”.
Akizungumzia suala la utendaji kazi, Mhe. Hapi, amewataka watumishi kutofanya kazi kwa mazoea bali kutimiza wajibu wao kwa ubunifu na uaminifu kwa mujibu wa kanuni, taratibu na sheria ili kuleta matokeo chanya kwa umma wanaoutumikia.
“Awamu ya tano inazungumzia hapa kazi tu, kwanza ni lazima mkiheshimu chama cha mapindizi maana serikali hii haikujileta yenyewe, pili, lazima watendaji mtoke ofsini na kwenda kuwahudumia wananchi ili kutatua shida zao, kutenda haki na kuwa waadilifu lakini pia ni lazima tuongeze juhudi za kukusanya mapato ya serikali kwa kubuni vyanzo vipya vya mapato ili Halmashauri zote za Mkoa wa Iringa zisishuke asilimia 90%”alisema Mhe Hapi.
Katika hatua nyingine, Mhe. Hapi amesema anatarajia kuanza kufanya mikutano ambapo kwa muda wa siku 18 atazunguka kwenye Halmashauri zote za Mkoa wa Iringa na kufanya mikutano isiyopungua mitatu kwenye kila Tarafa katika mikutano hiyo, atazungumza na wananchi sanjari na kusikiliza kero zao zoezi ambalo litaitwa Iringa Mpya.
Akisoma taarifa ya Wilaya, Mkuu wa wilaya Mufindi Mhe Jamhuri David William, amesema, anaishukuru serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Rais Dkt John Pombe Magufuli, kwa kuendelea kuleta fedha katika Wilaya yake.
Ameongeza kuwa, mwaka 2017/2018 Wilaya ya Mufindi ilipokea fedha kutoka serikali kuu kiasi cha Tsh Bilioni 06 na Milioni 200 kwa ajili ya maendeleo na matumizi ya kawaida.
Tarehe 28 Julai Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alimteua Mhe. Ally Hapi, Kuwa Mkuu wa Mkoa wa Iringa akirithi nafasi ya Mhe. Amina Masenza, aliyestaafu kwa mujibu wa sheria, awali Mhe. Hapi alikuwa Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni Jijini Dar es alaam.
Mkuu wa Mkoa Iringa Mh Ally Salum Hapi akiongea na Watumishi wa Wilaya ya Mufindi (Picha na Ofisi ya Habari Mwasiliano na Uhusiano Halmashauri ya Mufindi) .
|
Mkuu wa Mkoa Iringa akiongea na Watumishi wa Halmashauri ya WilayaMufindi |
Kaimu Chifu wa Wahehe akiongea na watumishi wa Wilaya ya Mufindi ikiwa ni Moja ya Ukaribisho wa RC Mpya Mufindi |
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya Mufindi Mhe Festo Mgina akitoa salamu za Shukrani kwa ujio wa Mkuu wa Mkoa |
RC-Iringa waliokaa (katikati) akiwa katika Picha Ya Pamoja na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya Mufindi |
|
No comments:
Post a Comment