Wednesday, June 20, 2018

Serikali kujenga hospitali 67 nchini

Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais -TAMISEMI Mh. Josephat Kakunda ameliambia Bunge kuwa ni azma ya serikali kujenga hospitali katika kila wilaya nchini kwa kuanzia na hospitali 67 zitakazoanza kujengwa zimekwishatengewa fedha.

Waziri Kakunda alikuwa akijibu maswali kutoka kwa wabunge juu ya uboreshaji wa sekta ya afya na ujenzi wa hospitali za wilaya katika maeneo ambayo hayana ambapo amesema serikali itaendelea kudumisha huduma za afya kadiri bajeti itakavyokuwa inaruhusu.

Kuhusu kupandishwa hadhi kwa kituo cha afya cha Sinza Palestina kuwa hospitali ya wilaya kama ilivyoahidiwa na serikali kituo hicho swali lililoulizwa na Mbunge wa Ubungo Saed Kubenea,Mh Kakunda amesema baada ya kufanya ukaguzi kituo  hicho hakiwezi kuwa kituo cha afya kutokana na changamoto ya eneo na kuielekeza halmashauri ya Ubungo kutenga eneo la ekari 25 kwaajili ya ujenzi wa hospitali ya wilaya.

Akiongezea katika majibu ya maswali hayo Waziri wa Afya Mh Ummy Mwalimu amesema serikali  imeamua kwa sasa kila halmashauri kuwa na hospitali ili kurahisha huduma kwa wananchi na tayari wameshaagiza kuanza kwa utekelezaji wa mpango huo.

 Chanzo:http://zanzibar24.co.tz/

Tuesday, June 19, 2018

Waziri Jafo awang'akia TBA kwa ukarabati mbovu Malangali Sekondari, aipongeza Halmashauri ya Mufindi

Waziri wa nchi Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI ) Mhe. Selemani Jafo, amewaagiza wakala wa Majengo TBA Mkoani Iringa, kurudia ukarabati wa sakafu za madarasa ya Sekondari kongwe ya Malangali baada ya kubaini kuwa imejengwa chini ya kiwango, huku akipongeza ujenzi wa kituo cha Afya Malangali unaotekelezwa na Halmashauri ya Wilaya ya Mufindi kwa mtindo wa ‘Force Account’

Waziri wa nchi TAMISEMI Selemani Jafo, akiwasili katika viwanja vya kituo cha Afya Malangali kukagua maendeleo ya ujenzi wa kituo hicho.
Waziri Jafo, ametoa agizo hizo wakati wa ziara ya kikazi katika Halmashauri ya Wilaya ya Mufindi, yenye lengo la kukagua maendeleo ya ujenzi wa kituo cha Afya Malangali, baada ya Ofisi ya Rais TAMISEMI kutoa shilingi milioni 400 za kutekeleza mradi huo.
Jafo, amesema yeye kama Waziri mwenye dhamana na Shule hapa nchini, hawezi kuvumilia anapoona Taasisi ya Serikali inatekeleza mradi chini ya kiwango wakati inalipwa mabilioni ya fedha za umma.
“Halafu mimi Jafo Shule zipo chini yangu unafikiri nitakubali “I never” ni bora mngeacha Sakafu ya kwanza, Taasisi ya Serikali ni lazima ifanye kazi ya Serikali kiusahihi na si kiujanja ujanja kama hivi, nenda mkaone Majengo ya Kituo cha Afya hapo jirani yaliyojengwa kwa Force account, Majengo ni mazuri yanaubora chini yamewekwa “tiles” alisema Waziri huku akigonga viatu vyake kwenye sakafu ambayo ilionesha vyufa kadri alivyokuwa akigonga.
Akijibu hoja za Waziri, fundi Mkuu wa TBA katika mradi huo Bi.Agnes Haule, amekili udhaifu wa ujenzi na kufafanua kuwa, sababu ya tatizo hilo linatokana na uamuzi wa kusakafia kabla ya kukauka kwa zege kutokana na uhitaji wa vyumba vya kusomea na kuongeza kuwa wapo tayari kurudia kazi hiyo.
Awali akikagua maendeleo ya ujenzi wa kituo cha Afya Malangali, unaotekelezwa kwa mfumo wa force account kwa kutumia mafundi wenyeji Mh. Jafo, amefarijika na maendeleo ya ujenzi huo kwa kuwa umezingatia viwango na thamani ya fedha.

Kazi hii inamaanisha kwamba tunauongozi mzuri wa Halmashauri ya Mufindi na Wilaya nzima ya Mufindi na hakikisheni mnamaliza kazi hii ikiwa salama, nimeangalia vitu mbalimbli, kuta zenu na ujenzi kwa ujumla mko vizuri. Aidha, mnavyofanya vizuri mnatushawishi zaidi kwamba siku nyingine tunapokuwa na mradi, tuifikirie Mufindi kwanza na haya ndiyo mambo ambayo Mheshimiwa Rais anataka kuyaona na si vinginevyo”
Mnamo mwezi wa 12/ 2017, Halmashauri ya Mufindi ilipokea kiasi cha shilingi milioni 400 kutoka Ofisi ya Rais TAMISEMI ili zitumike kufanya utanuzi wa kituo cha Afya Malangali unaojumuisha, Nyumba ya Mganga, Maabara, Chumba cha upasuaji na Wodi ya Mama na Mtoto na ujenzi wake ulianza rasmi mwezi 01/2018 na unatarajiwa kukamilika mwishoni mwa mwezi huu wa 06.
Waziri nchi TAMISEMI Mhe. Selemani Jafo, akikagua  maendeleo ya jengo la maabara

Monday, June 4, 2018

MKUU WA WILAYA MUFINDI AWATAKA WAZAZI KUCHANGIA CHAKULA SHULENI.





 Mkuu wa Wilaya ya Mufindi amewataka wazazi na walezi waendelee kuchangia chakula cha mchana kwa wanafunzi wa kutwa kwa shabaha ya kuinua kiwango cha ufaulu, kupunguza utoro pamoja na kuleta usawa miongini mwao.

Akiongea na wananchi wa Igowole katika kilele cha wiki la kusoma  lililofanyika katika Viwanja vya shule ya Msingi Igowole iliyopo Halmashauri ya Wilaya Mufindi, Mwakilishi wa Mkuu wa Wilaya ya Mufindi Bwana Joseph Mchina, amewataka vingozi wa serikali za vijiji kuendelea kutekeleza mkakati wa utoaji wa chakula cha Mchana shuleni kwa kuwamasisha wazazi kuchangia kwa mujibu wa sera ya Elimu bila malipo.

Aidha, amewapongeza viongozi wa siasa ambao wamekuwa bega kwa bega katika kuelimisha jamii na wazazi kuhusu umuhimu wa utoaji wa chakula cha mchana shuleni.

 Napenda kupongeza kata zote ambazo zinazotoa chakula cha mchana kwa wanafunzi shuleni, utoaji wa chakula cha mchana shuleni huleta usawa kati ya walionacho na wasionacho, huimarisha mahudhurio ya wanafunzi shuleni huongeza usikivu wa wanafunzi darasani na hutunza muda wa ratiba nzima ya shule” alisema Mchina

Akitoa taarifa kwa mgeni rasmi, Afisa Elimu wa Halmashauri ya Wilaya ya Mufindi Bwana Kennedy Bukagile, alisema Halmashauri ya Wilaya Mufindi imejiwekea mkakati mzuri wa kuwapatia wanafunzi chakula cha mchana ili kuimarisha usikivu  na mahudhurio shuleni,

 wazazi wamejitoa kulima shamba la maharage na Mahindi lenye jumla ya hekari 294 kwa ajili ya chakula cha mchana kwa wanafunzi shuleni”        
            
Afisa huyo mwenye dhamana ya Elimu, ameongeza kuwa, Idara yake kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wamewezesha kamati za shule kujengewa uwezo wa uhamasishaji na pia kuwa na wahamasishaji jamii  wa masuala ya  elimu kwa kila shule, wakishirikiana na kamati za shule kuhakikisha kuwa wanafunzi wanapata chakula cha mchana jambo ambalo limesabisha kuongezeka kwa ufaulu sanjari na kushuka kwa takwimu za utoro.

Kwa upande mwingine Maadhimisho hayo yalienda sambamba na maonesho ya mabanda ya elimu na mashindano ya wanafunzi katika stadi za KKK, ambapo washindi wa shindano hilo walitangazwa na kupewa zawadi na Mgeni rasmi ambapo nafasi ya kwanza ilichukuliwa na Mwanafunzi Anania Ng’umbi, darasa la pili wa Shule ya Msingi Igowole.

Aidha “kujua kusoma na kuandika ni haki ya kila mtu jambo hilo linamsaidia mtu kuwa na uwezo na njia yenye kumuwezesha kufanya maendeleo katika maisha yake pamoja na watu wengine”, Tamko la Shirika la UNESCO

Maadhimisho ya Wiki la Kusoma yanalenga kukuza na koungeza ari ya ushindani katika kujifunza stadi za msingi za kusoma, Kuandika na Kuhesabu (KKK) Ujumbe wa wiki la elimu mwaka huu ni Stadi za KKK ni Msingi wa Elimu, tuwekeze katika Elimu kuelekea Uchumi wa Viwanda